Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko alipokutana na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Rashal Energies, Farhiya Warsame,
Kampuni hiyo pia itajenga vituo vitano vya CNG kwa ajili ya kujaza gesi kwenye magari na viwanda huku ikiwa na lengo la kufikisha zaidi ya vituo 30.
Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam wakati wa Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25) yanayofanyika kwa siku tatu jijini humo.
Dkt. Biteko amesema kuwa lengo la serikali ni kuwa na mtandao mkubwa wa mabomba ya gesi pamoja na vituo vya kujazia gesi kwenye magari ili kuwezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi.
Aliongeza kuwa Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano kwa kampuni zinazotaka kuwekeza katika kutoa huduma hii kwa wananchi.
Kwa upande wake, Farhiya Warsame alitoa shukrani kwa Dkt. Biteko kwa miongozo yake ambayo imesaidia kampuni hiyo kuanza kutekeleza mradi huo.
Alilishukuru pia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla kwa jitihada kubwa katika kuhakikisha mradi huo unakamilika.
Rashal Energies ni kampuni yenye makao makuu jijini Dar es Salaam inayomilikiwa na kuendeshwa na Watanzania wazawa, huku ikiajiri wataalam kutoka nchini Tanzania.
Kampuni hiyo imefanya utafiti wa kina kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi huo, na imefuata taratibu na sheria zote za nchi ikiwa ni pamoja na kupata vibali vyote vinavyohitajika.
Akizungumzia mradi huo, Farhiya alisema kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Kisemvule, wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani, lenye urefu wa kilomita 19 hadi Mbagala Rangi Tatu, kutakuwa na kituo cha Rashal Energies cha kujaza gesi kwa magari, ikiwa ni pamoja na kuhudumia mabasi ya mwendo kasi.
“Rashal Energies pia itajenga vituo zaidi ya 30 vya kujaza gesi asilia, mtandao wa mabomba ya gesi kwa ajili ya magari, bajaji, na pikipiki, pamoja na kusambaza gesi viwandani,” alisema, Farhiya.
Katika kipindi cha ujenzi wa bomba hili, inatarajiwa kuanzishwa ajira zaidi ya 300 za moja kwa moja, na zaidi ya 200 zitapatikana baada ya kukamilika kwa vituo zaidi ya 30 vya gesi asilia (CNG) jijini Dar es Salaam.
Ili kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rashal Energies itaanzisha huduma ya kujaza gesi kwa matumizi ya majumbani ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.
Baada ya kukamilika kwa utafiti, sasa kampuni inaenda mbele na kuanzisha mradi huu kwa madhumuni ya kusambaza gesi ikiwa ni njia mbadala ya nishati safi ili kulinda mazingira.