Friday , 7th Mar , 2025

Wakati dunia ikiendelea kumuombea afya njema kiongozi wa Kiroho Papa Francis leo ametuma ujumbe wa sauti kwa mara ya kwanza na kuwashukuru wote wanaoendelea kumuombea

Katika ujumbe wake wa kwanza kupitia kutuma sauti tangu alipolazwa hospitalini tarehe 14 mwezi Februari, Papa Francis wa kanisa la katoliki amewashukuru wale ambao wamekuwa wakimuombea afueni ya haraka.

Papa Francis mwenye umri wa miaka 88 amekuwa hospitalini kwa takriban wiki tatu baada ya kuugua homa ya mapafu.

Katika ujumbe mfupi wa sentensi mbili kutoka hospitali ya Gemeli alikolazwa, Papa amesikika kupumua kwa taabu wakati akiwashukuru wasamaria wema kwa dhati.

Ujumbe huo ulichezwa wakati wa ibada ya usiku ya kumuombea Papa katika kanisa la St Peter's Square iliyoko Vatican.

Hata hivyo, Vatican imesema ujumbe huo ulirekodiwa jana Alhamisi.

Hivi karibuni, Vatican ilitangaza kuwa Papa alikuwa katika hali ya utulivu baada ya kushuhudia matukio mawili ya kushindwa kupumua, na alikuwa akitumia msaada wa “mashine ya kupumua,” lakini sasa amerejea kutumia maski ya oksijeni.

Papa amekuwa akilazimika kutohudhuria shughuli kadhaa tangu kupelekwa hospitalini, ikiwa ni pamoja na ibada ya Jumatano ya Majivu, ambayo inaashiria mwanzo wa kipindi cha majuma sita kuelekea Pasaka.