Sunday , 2nd Mar , 2025

Waziri wa Afya Jenista Mhagama , amesema hospitali maalum ya tiba magonjwa ambukizi Kibong'oto inatarajiwa kuwa taasisi ya magonjwa ambukizi ambayo itakwenda sambamba na uimarishaji wa mifumo ya huduma za tiba ya magonjwa hayo.

Waziri wa Afya alipotembelea ospitali maalum ya tiba magonjwa ambukizi Kibong'oto

Waziri Mhagama amesema hayo alipofanya ziara katika Hospitali ya Kibong'oto kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo serikali imetoa fedha ikiwa ni pamoja na eneo la uzalishaji wa gesi tiba na ununuzi wa mashine za kisasa za kuchomea taka.

"Tumejipanga kwenye sekta ya afya, pamoja na huduma nyingine za afya za kibobezi, tunataka kuuthibitishia ulimwengu kwamba hata kwenye eneo hili la magonjwa ambukizi kama nchi tumejidhatiti vizuri kwa kuhakikisha mifumo yetu ya tiba iko imara," amesema

Waziri Mhagama. "Kwahiyo hapa sasa kitakuwa ni kituo cha umahiri katika eneo hilo la magonjwa ambukizi, nina furahi nilipokuja kuzindua bodi tulikubaliana ni lazima tuwe na mpango mkakati unaotekelezeka, ambao utatufikisha kwenye malengo endelevu na sasa naona utekelezaji wake umeanza," amesema Waziri Mhagama. 

Aidha Waziri Mhagama amesema Serikali imewekeza zaidi zaidi ya shilingi milioni 550 kwa ajili ya kujenga sehemu maalum ya kuchomea taka pamoja na ununuzi wa mashine maalum ya kisasa ambayo ina uwezo wa kuteketeza taka zaidi ya Kg 400 kwa saa moja katika eneo hilo.