Tuesday , 25th Feb , 2025

Jeshi la Polisi mkoani Geita limesema kwamba wanafunzi saba wa kidato cha sita, katika shule ya Sekondari ya Geita (GESECO) wamefukuzwa shule baada ya kukutwa na hatia ya kuhamasisha vurugu zilizofanyika shuleni usiku wa Februari 20, 2025.

Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) Safia Jongo

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) Safia Jongo ametoa taarifa hiyo na kuongeza kuwa wanafunzi 19 wamesimamishwa shule hadi Mei 05, 2025 huku wanafunzi wengine 45 wakisimamishwa shule kwa muda wa siku 21.

Kamanda Jongo amesema kabla ya hatua hiyo, Februari 21, 2025 Jeshi la Polisi liliwashikilia wanafunzi 30 wa kidato cha sita wa shule ya sekondari iliyopo Manispaa ya Geita kwa tuhuma za kufanya vurugu shuleni hapo.

Amesema mbali na wanafunzi 30 walioshikiliwa pia wengine 41 walijumuishwa na kufanya jumla ya wanafunzi waliohojiwa kuwa 71 ambapo uchunguzi umekamilika kwa kushirikiana na bodi ya shule.

Kamanda Jongo ameeleza kati ya wanafunzi hao 71 waliobainika kuhusika kwenye tukio hilo, wanafunzi saba wamefukuzwa shule baaada ya kukutwa na hatia ya kuhamasisha vurugu hizo.