
Wakati mzozo ukiendelea katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambayo inapakana na Burundi, zaidi ya watu 10,000 wamekimbilia nchini Burundi, Wizara ya Mambo ya ndani ya Burundi imethibitisha kuwa mpaka sasa Burundi tayari inahifadhi jumla ya wakimbizi zaidi ya 86,000 kutoka DRC
Katika mkutano na waandishi wa habari, Waziri Martin Niteretse alisema kuwa wengi wao wamewasili katika siku tatu zilizopita. "Tangu Jumapili tarehe 14 hadi Jumapili Februari 16, Burundi imepokea karibu wakimbizi 10,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo," amesema Niteretse.
Wakimbizi hao wanavuka Mto Rusizi upande wa Cibitoke au kupitia Uvira, eneo la DRC lililo karibu na Gatumba nchini Burundi.
Kwa mujibu wa waziri huyo, wakimbizi watapelekwa katika kambi za muda za Cibitoke na Gihanga katika mkoa wa Bubanza, Hata hivyo baadaye watapelekwa katika kambi za wakimbizi zilizo mbali na mpaka kama vile Rutana na Ruyigi mashariki mwa nchi.
Amema kwa sasa kuna juhudi za kuwatenganisha raia wa kawaida, wanajeshi, na wale walio na matatizo ya kiafya.