Wednesday , 12th Feb , 2025

Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limemkamata John Kandole (11), mwanafunzi wa darasa la 7 katika shule ya Msingi Lwemba kwa tukio la kujaribu kumuua mama yake mzazi aitwaye Regina John Kalinga (44) kwa kuweka sumu kwenye chakula kisa tu anachukizwa na tabia ya mama yake ya kupenda kumtuma.

Wali maharage

Taarifa hiyo imetolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro na kusema tukio hilo limetokea Februari 11, 2025 mchana katika kitongoji cha Msalabani juu, kijiji cha Iwemba, kata ya Kidodi, Tarafa ya Mikumi, wilaya ya kipolisi Ruhembe (Kilosa), Mkoa wa Morogoro, baada ya kijana huyo kuweka sumu aina ya Lara force ambayo hutumika kuua wadudu kwenye mbogamboga, ambayo iliwekwa kwenye mboga aina ya maharage yaliyoliwa kwa pamoja na wali ambao ulipikwa na mama yake mzazi.

"Baada ya kula chakula mama huyo na watu wengine watano walianza kuumwa sana na tumbo na kukimbizwa hospital ya St. Kizito ambapo amelazwa akiendelea na matibabu, Watu wengine watano wametibiwa na kuruhusiwa ambapo wamefahamika kuwa ni Eusebia Kamili (53), Zena Salehe (17), Patrick Ndola (11), Alvin Alex (5) na Hidaya Swedi (1),"

"Uchunguzi wa awali umebainisha kuwa chanzo cha tukio hilo ni kwamba mtoto huyo anachukizwa na tabia ya mama yake ya kumtuma tuma na kumpangia kazi nyingi na kumnyima muda wa kucheza na wenzake," imeeleza taarifa hiyo.