Wednesday , 18th Mar , 2015

Serikali ya India imekubali kuipatia Tanzania dola za Marekani milioni 100 kwa ajili ya kuongeza maji katika Jiji la Dar Es Salaam na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani, ambako kwa sasa unakamilishwa mradi mkubwa wa kuwaongezea maji wakazi wa jiji.

Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umma la India ambalo linashughulikia miradi ya maji na umeme la WAPCOS, R.K Gupta.

Katika awamu nyingine ya uvutaji maji kutoka Ziwa Victoria, Serikali vile vile inakusudia kuanza mazungumzo na Serikali ya India kwa ajili ya kupatiwa mkopo ambao utapeleka maji katika miji ya Magu, Bariadi, Maswa, Kishapu na Mwanuhuzi katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Simiyu.

Aidha Serikali imekamilisha mipango ya kuvuta maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya wakazi wa mjini ya Tabora, Nzega na Igunga katika Mkoa wa Tabora.

Mipango hiyo mikubwa mitatu ya kuongeza upatikana wa maji kwa wananchi ilielezwa wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipokutana na kuzungumza na Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umma la India ambalo linashughulikia miradi ya maji na umeme la WAPCOS.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa WAPCOS, Bwana R.K. Gupta amemweleza Rais Kikwete kuwa India imekubali kugharimia mradi huo na iko tayari kusaini mkataba na Tanzania ambako Serikali hiyo itatoa mkopo wa dola za Marekani zinazokaribia milioni 280 kwa ajili ya kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria kwenda mjini ya Tabora, Nzega na Igunga katika Mkoa wa Tabora.

Pamoja na kumshukuru binafsi Gupta na Serikali ya India kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali yake katika sekta ya maji, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania iko tayari wakati wowote kutia saini makubaliano ya kuwezesha kupatikana kwa fedha za kusambaza maji katika miji hiyo mitatu.

Uvutaji maji huo utakuwa ni awamu ya pili, baada ya Serikali kukamilisha uvutaji maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya wakazi wa mjini ya Shinyanga na Kahama ambao sasa wanapata maji safi na salama na kwa kiasi cha kutosheleza kutoka Ziwa hilo.

Rais Kikwete amemweleza Bwana Gupta kuwa pamoja na kwamba Serikali inakamilisha mradi mkubwa wa kuongeza upatikanaji maji katika mikoa wa Dar Es Salaam na Pwani, bado zinahitaji juhudi zaidi ili kuhakikisha kuwa wakazi wote wa Mikoa hiyo miwili wanaongezewa maji safi na salama.

Bwana Gupta amesema kuwa Serikali ya India iko tayari kutoa kiasi cha dola za Marekani milioni 100 ili kufanikisha ongezeko la maji katika maeneo hayo ya Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.
Kuhusu miji ya Magu, Bariadi, Maswa, Kishapu na Mwanuhuzi, Gupta pia ameelezea utayari wa Serikali yake kutoa fedha za kujenga miundombinu ya kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika miji hiyo iliyoko Kanda ya Ziwa Victoria.

Bwana Gupta ameishauri Serikali ya Tanzania kuwasilisha ombi rasmi kwa Serikali ya India ambayo ameonyesha mwelekeo mkubwa kuwa inaweza kutoa fedha za kujenga miundombinu hiyo.