Wednesday , 29th Jan , 2025

Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango, amesisitiza umuhimu wa kubuni mifumo na mbinu za kutunza vyanzo vya maji na ardhi oevu, akieleza kuwa matumizi ya maji kwa binadamu, mifugo, na wanyamapori yanapaswa kuzingatiwa kwa usawa.  

Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango

Akizungumza wakati akifungua Kongamano la Nne la Kimataifa la Kisayansi la Maji, Januari 29, 2025, katika Ukumbi wa Mlimani City, Dkt. Mpango amewataka wataalamu wa sekta ya maji, hususan wa Chuo cha Maji, kutumia teknolojia ya Akili Mnemba (AI) katika kutafuta suluhisho la changamoto za maji na usafi wa mazingira.  

"Ninawaomba, hasa wenzetu wa Chuo cha Maji, tumieni Akili Mnemba (AI) kila inapowezekana katika kutafuta suluhisho la changamoto za maji na sanitation. Pia mshirikishe vijana bunifu wa Kitanzania na nchi zingine za Afrika," amesema.  

Ameeleza kuwa tafiti na ubunifu vinapaswa kuimarisha uelewa wa pamoja kuhusu uhaba wa rasilimali za maji ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.  

Akizungumzia kaulimbiu ya kongamano hilo, "Suluhisho la Changamoto za Maji na Uondoaji wa Maji Taka Katikati ya Mabadiliko ya Tabianchi," Dkt. Mpango amesema serikali imejipanga kushirikiana na wadau mbalimbali kwa kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya maji kupitia mamlaka za mabonde kama Rufiji na Wami-Ruvu, pamoja na kushiriki katika taasisi za kimataifa kama Bonde la Mto Nile na Ziwa Tanganyika.  

Kwa upande wake Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema serikali imekubaliana kuhakikisha kila mradi wa maji vijijini unakuwa na mtaalamu maalum wa kuhudumia miundombinu yake. 

"Katika kila mradi vijijini lazima awepo mtaalamu, kwa maana ya technician, ambaye amezalishwa ndani ya Chuo cha Maji," ameongeza.  

Kongamano hilo limewaleta pamoja wataalamu wa sekta ya maji kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujadili changamoto na kutafuta mbinu za kuboresha upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira nchini.