Marais 20 wa Afrika wameshiriki Mkutano wa Nishati unaoendelea leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Rais wa Liberia, Joseph Boakai ndiye kiongozi wa 19 kuwasili nchini kuungana na viongozi wengine katika Mkutano huo mkubwa kufanyika nchini.
Katika mkutano huo, pia umeshuhudia Rais wa Benki ya Dunia, Ajay Banga akitembelea Tanzania kwa mara ya kwanza
RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania ni moja kati ya nchi 12 zitakazozindua mpango mahususi wa kitaifa kuhusu nishati ambapo kupitia mpango huo unatarajia kuongeza kasi ya kuunganisha umeme nchini hadi kufikia asilimia 72 ifikapo mwaka 2030.
“Ili kufanikisha azma hiyo ndani ya muda wa miaka mitano ijayo, tutahitaji uwekezaji wenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 13, ambapo dola bilioni 5 zitapatikana kutoka sekta binafsi hapa nchini,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema hayo leo wakati akizungumza kwenye Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi Afrika unaoendelea muda huu ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.