Wednesday , 15th Jan , 2025

Ikiwa zimebaki siku 3 kwa huduma ya TikTok kuziwa rasmi nchini Marekani, kubwa na mpya kwa sasa ni ujio wa mbadala wa TitTok kitu ambacho kimewashangaza walio wengi.

 

Wakati mvutano unaendelea kati ya kampuni ya Bytedance inayomiliki mtandao wa TikTok na serikali ya Marekani juu ya uwezekano wa kuzuia moja kwa moja upatikanaji wa huduma za mtandao huo nchini humo au kuuza kampuni hiyo kwa wawekezaji kutokea nchini Marekani, kubwa liloshangaza wengi ni kuibuka kwa application ya RedNote ambayo pia inamilikiwa na wawekezaji wa kutokea China.

Kwa ufupi RedNote inavyofanya kazi kimatumizi ni kama vile TikTok ila hii yenyewe imeongezewa huduma ya picha na inafahamika zaidi kama soko huru ambalo wafanyabiashara huweka bidhaa na watu huwezeshwa kununua au kuandika kitu kuhusu bidhaa hiyo.

Sasa baada ya taarifa ya huduma za mtandao wa TikTok kusitishwa ifikapo tarehe 19 mwezi huu, nusu ya watumiaji wapya zaidi ya 500,000 kutokea nchini Marekani wamejiunga na mtandao huu huku baadhi ya watumiaji hao wameonekana wakiuliza vitu mbalimbali kuhusu nchi ya China ikiwemo vyakula na vichekesho vinavyofanya vizuri nchini huko.

Sasa ule msemo wa baniani mbaya kiatu chake dawa ndiyo unakuja hapa sasa, kwani kinachofanya serikali ya Marekani kuzuia huduma za TikTok nchini humo ni sababu za kiusalama kwa kudai kuwa mtandao huo unamilikiwa na China hivyo kwa upande wao si njema sana ukizingatia ushindani wao kiuchumi.

Pili na ajabu zaidi mtandao wa RedNote unamilikiwa na kampuni ya China pia ambayo inafahamika kama (Xingin Information Technology) na hadi sasa kwenye soko la Appstore kwa nchini Marekani ndiyo application ambayo inapakuliwa kwa kasi zaidi na baadhi ya wahamiaji waliotokea kwenye mtandao wa TikTok

Mtihani ni kwamba serikali ya Marekani watahitaji kununua mtandao wa RedNote pia? au watazuia matumizi kabla ya idadi ya watumiaji haijawa kubwa zaidi? kwa maana TikTok kwa Marekani ina watumiaji zaidi ya milioni 170, wacha tuone itakavyokuwa.