Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akikata utepe kwenye jengo la kituo cha Afya
Akihutubia jana Ijumaa wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kituo kipya cha Afya Kizimkazi, katika Wilaya ya Kusini Unguja, Dkt. Kikwete alisisitiza kuwa mafanikio hayo, ambayo ni dhahiri kwa kila mmoja, yanapaswa kupongezwa na kuenziwa.
Uzinduzi wa kituo hicho ni mojawapo ya matukio muhimu katika kusherehekea miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ambayo kilele chake kitakuwa tarehe 12 Januari 2025.
Dkt. Kikwete alibainisha kuwa kituo hicho cha kisasa kina uwezo mkubwa wa uchunguzi wa maradhi na tiba, hivyo ni mkombozi wa huduma za afya kwa wakazi wa Kizimkazi na maeneo jirani.
Alihimiza umuhimu wa kutunza majengo na vifaa vya kituo hicho ili kuhakikisha huduma hizi za thamani zinadumu kwa muda mrefu, "Tukitunze kituo kidumu; ni chetu, ni mali yetu, ni kwa ajili yetu sote", alisisitiza Dkt. Kikwete.
Rais Mstaafu aliambatana na mkewe, Mama Salma Kikwete, ambaye ni Mbunge wa Mchinga, pamoja na viongozi wengine wa kitaifa. Hafla hiyo ilihudhuriwa na mamia ya wananchi wenye furaha kubwa.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, Kituo cha Afya Kizimkazi kinatarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 13,000 kutoka shehia za Kibuteni, Kizimkazi Mkunguni, na Kizimkazi Dimbani, pamoja na maeneo jirani kama Muyuni.
Katika mwaka 2024 pekee, jumla ya watu 12,389 walihudumiwa kituoni hapo, wakiwemo wanaume 5,068 na wanawake 7,325.
Kituo hiki kimejengwa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali, wakiwemo Samia Foundation, Foundation for Humanitarian Initiatives ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Benki ya NBC, pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.