Wednesday , 18th Dec , 2024

Askari Polisi wawili wa wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, wamefariki dunia usiku wa kuamkia leo Desemba 18, 2024, katika majibizano ya risasi kati yao na mtuhumiwa wa ujambazi baada ya kufika nyumbani kwake kwa ajili ya kumkamata.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi George Katabazi,

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi George Katabazi, amesema mtuhumiwa huyo naye alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa mapambano hayo.

"Askari Polisi wawili walifariki dunia katika mapambano ya risasi na mtuhumiwa, Askari Polisi hao wakiwa na wenzao walipata taarifa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa anatafutwa na yupo nyumbani kwake katika kijiji cha Msagali, ambapo walifika kijijini hapo na kuukuta uongozi wa kijiji hicho na kuelekea nyumbani kwa mtuhumiwa huyo, mtuhumiwa alitoka ndani ya nyumba na kuanza kuwashambulia Askari na katika majibizano ya risasi na ndipo vikatokea vifo vya watu watatu. Aidha katika majibizano hayo Askari mmoja na raia mmoja walijeruhiwa na wanaendelea na matibabu," amesema Kamanda Katabazi.