Thursday , 24th Oct , 2024

Mkuu wa mkoa Dar es Salaam Albert Chalamila amewaagiza madaktari na wauguzi wa hospitali za serikali kuondoa vizingiti kwa wagonjwa wanaokwenda kutibiwa kwenye hospitali hizo ili kuondoa taswira mbaya kwenye sekta hiyo.

Hayo yameelezwa katika ziara ya usiku inayoendelea katika mkoa wa Dar es Salaam ambapo usiku wa kuamkia hii leo ikiwa ni zamu ya Wilaya ya kinondoni ambapo mkuu wa mkoa ametembelea hospitali ya wilaya hiyo ambapo amesema huduma mbovu zinazopotelewa katika hospitali za serikali zinapelekea maneno na kashfa na dhihaka mitandaoni.

“Wagonjwa wakija hapa mara tatu mara nne wakakutana na vizingiti mbalimbali vya kihuduma, matusi na yanaenda kwa serikali kwa hiyo sisi tuna wajibu wa kupunguza kejeli na dhihaka kwa serikali na mheshimiwa rais dhidi ya huduma mbovu zinazotolewa baadhi ya maeneo yetu ambayo tunayafanyia kazi na sekta ya afya ni sekta muhimu na madaktari mlio hapa sekta hii haihitaji siasa na katika sekta ambayo msije mkalogwa mkaingiza siasa ni sekta ya Afya” Amesema Albert Chalamila.

Aidha pia amewahasa wauguzi kutumia lugha nzuri pindi wanapo hudumia wagonjwa na kutowachangisha wananchi gharama za matibabu na pindi inapobidi mgojwa kuchangia huduma basi aelekezwe kwa utaratibu na kama hana uwezo basi wasilazimishe waone namna ya kuweza kuwasaidia wagonjwa hao.