Tuesday , 22nd Oct , 2024

Serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa daraja la Jangwani lenye urefu wa mita 390 na barabara za maungio zenye urefu wa mita 700 katika barabara ya Fire - Ubungo kwa gharama ya Shilingi Bilioni 97.1 ambapo kazi ya ujenzi itatekelezwa kwa miezi 24. 

Mkataba huo umesainiwa leo Oktoba 22, 2024 Mkoani Dar es Salaam kati ya Wakala ya Barabara (TANROADS) na Mkandarasi wa Kampuni ya China Communications Construction Company Limited na kushuhudiwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa na viongozi wengine.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini huo, Waziri Bashungwa ameeleza kuwa ujenzi wa daraja hilo utaondoa kero kwa wananchi na adha ya usafiri kutokana na eneo hilo kujaa maji mara kwa mara na kusababisha barabara kufungwa na kutopitika mvua zinaponyesha.

Bashungwa amemuelekeza Mkandarasi huyo kukamilisha maandalizi na kupeleka vifaa na mitambo ndani ya miezi mitatu katika eneo la Jangwani ili kazi iweze kuanza na kuhakikisha anajenga haraka kwa mujibu wa usanifu na mkataba kama ilivyopangwa.

Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa ujenzi wa daraja hilo utaenda sambamba na ujenzi wa kingo za Mto Msimbazi ambao utatekelezwa na Ofisi ya Rais - TAMISEMI ikiwa ni katika programu ya uendelezaji wa Bonde la Msimbazi.