Saturday , 7th Sep , 2024

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Watanzania wanaoishi nje ya Nchi (Diaspora) kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana katika sekta mbalimbali nchini.

Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan akiwa na baadhi ya Watanzania waishio China

Rais Samia ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na Diaspora waishio nchini China katika mkutano uliojumuisha watanzania wanaofanya kazi nchini humo, wafanyabiashara na wanafunzi uliofanyika jijini Beijing tarehe 6 Septemba 2024. 

Akizungumza na Diaspora hao waliojitokeza kwa wingi, wakionesha furaha na shauku kubwa ya kuzungumza na Rais Samia, aliwaeleza kuwa licha ya fursa lukuki za kiuchumi zilizopo nchini Serikali imefanya maboresho ya sera na sheria mbalimbali ili kutoa fursa na kutanua wigo kwa Diaspora kuwekeza nchini.
 

Rais Samia amezitaja fursa hizo zinazopatikana katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi, viwanda, kilimo na madini. Aliongeza kufafanua kuwa, katika sekta ya ujenzi hivi sasa Serikali imeandaa utaratibu mahususi kwa Diaspora, unaowapa fursa ya kujengewa na kumiliki nyumba nchini. 
 

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwaeleza Diaspora kuhusu hatua liyopigwa na Serikali katika kuboresha utoaji huduma za kijamii kwa Wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, na usafirishaji akitolea mfano wa treni iendayo kwa haraka (SGR) ambayo katika kipindi kifupi imeleta mageuzi makubwa kwenye sekta hiyo na ujenzi wake ukiwa unaendelea. Sekta zingine ni nishati, kilimo, maji, mawasiliano na ukuaji wa demokrasia.

 

“Nyumbani tuko vizuri, mfano sasa hivi safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma inachukua saa 3 hadi 4 pekee kwa kutumia treni yetu mpya tuliyoizindua hivi karibuni. Tumefanya maboresho makubwa ya sera na sheria ili kuwapa fursa ya kuendesha shughuli za kiuchumi kwa urahisi. Njoeni muwekeze nymbani”. Alisema Rais Samia.

 

Mbali na hayo amepongeza juhudi na uzalendo unaoendelea kuonyeshwa na Diaspora  katika kuchangia shughuli za maendeleo nchini ikiwemo kuleta watalii, wawekezaji na kusaidia kuratibu shughuli za matibabu. Aliongeza kusema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la fedha zinazotumwa nyumbani (remittance) kutoka ughaibuni,

 

Vilevile, Rais Samia ametoa wito kwa Diaspora wa nchini humo na kwa nchi zingine, hususan kwa jamii ya wanafunzi kujiandisha katika vyama vyao vya Jumuiya kwenye maeneo waliyopo. Akasisitiza kuwa hatua hiyo hiyo, licha kusadia kutambuana na kukuza umoja wao inarahisisha namna ya kuwafikia wanapohitaji huma mbalimbali hasa wakati zinapotokea changamoto ikiwemo majanga kama vile mlipuko wa magonjwa.