Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango akiteta jambo na Waziri wa Madini
Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo leo Agosti 22, 2024, katika eneo la Mpwayungu wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma wakati akihitimisha ziara ya siku nne mkoani humo.
"Mwenyezi Mungu ametujaalia rasilimali hii ya madini mkakati yenye mahitaji makubwa sana duniani, Mkoa wa Dodoma umebarikiwa kuwa na madini haya mkakati kwa uwingi na aina tofauti tofauti, lazima rasilimali hii ikatafsirike katika maendeleo ya wananchi wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla Wizara ya Madini hakikisheni mnaweka mpango mzuri wa usimamizi wa rasilimali hii kwa manufaa ya Taifa na kwa manufaa ya vizazi vijavyo," amesema Dkt Mpango
Akiwasilisha salamu za Wizara,Waziri wa Madini Anthony Mavunde amemuahidi Dkt. Mpango kuyafanyia kazi maelekezo yote na kwa sasa Wizara inakamilisha andiko la mkakati wa usimamizi na uvunaji wa madini hayo ili yalete faida kwa nchi kwa kuchochea uchumi na kuendeleza sekta ya madini.
Waziri Mavunde alitumia fursa hiyo kutoa maelekezo kwa Afisa Madini Wakazi(RMOs) kuhakikisha wanasimamia ipasavyo maeneo yenye uchimbaji wa madini mkakati ili manufaa yake yaonekane kwa Taifa.