Friday , 9th Aug , 2024

Mamlaka ya Mapato nchini TRA, imekuja na mfumo wa SIKIKA APP, utakaowezesha Wafanyabiashara kutoa maoni au malalamiko yao moja kwa moja kwa Kamishna Mkuu wa mamlaka, ili kuboresha huduma na kupunguza changamoto zilizokuwa zinawakabili walipa kodi.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Mwenda.

Mfumo huo umelenga kuimarisha ushirikiano na mahusiano baina ya walipa kodi pamoja na mamlaka ili kuondoa malalamiko waliyokuwa wanakutana nayo walipa kodi na hapa Kamishna mkuu  wa TRA, Yusuph Mwenda, anafafanua zaidi.

“Tumejipanga kuimarisha mahusiano na walipa kodi lakini pia kutoa Elimu ya ulipaji kodi kwa kila mtanzania lakini kupitia mfumo huu unaweza kumripoti moja kwa moja mtumishi wa TRA asiye mwaminifu na sisi tutamshughulikia kwa mujibu wa taratibu zetu”, alisema Mwenda.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Tehama wa TRA, Emmanuel Nnkyo anasema mfumo huo utakuwa na usiri hivyo watumiaji wasiogope kutoa malalamiko yao.
“Mfumo huu una usiri mkubwa kwani utatuma maoni yako lakini utambulisho wako hautajulikana na utawasiliana moja kwa moja na Kamishna”, Alisema Nnkyo.

Kwa upande wao Wafanyabiashara wameomba malalamiko yatakayotolewa yaweze kufanyiwa kazi.
“Tuwapongeze mfumo ni mzuri na umelenga kutatua changamoto za Wafanyabiashara na sisi tuombe wasiishie tu kwenye kuyasoma badala yake wayafanyie kazi ndipo mfumo utaleta maana”, alisema Award Mpandilah.

“Mfumo utaleta uwazi kwenye kushughulika na changamoto na watajua nini hasa kilio cha wananchi, tunaomba pia wazingatie makadirio ya kodi yaendane na biashara zinazofanywa”, alisema Elias Marwa.