Friday , 19th Jul , 2024

Serikali imelitaka Baraza la michezo la Taifa Tanzania (BMT) kuhakikisha vyama vya michezo vinaleta mipango yao mapema kwa ajili ya kujiandaa na michezo ya Olimpiki ya Los Angeles 2028 itakayofanyika nchini Marekani.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo Dokta Sulemani Serera  katika hafla ya kuaga na kukabidhi bendera  timu ya Tanzania itakayoshiriki michezo ya Olimpiki itakayoanza Julai 26 mpaka Agosti 11 mjini Paris nchini Ufaransa.

"Mwaka huu tunawakilishwa na wachezaji saba  lengo letu ni kuona mwaka 2028 tunapeleka idadi kubwa ya wachezaji na Serikali itaendelea kushirikiana na Mashirikisho ya Michezo ili kufikia malengo yetu, amesema  Serera.

Upande mwingine,Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Filbert Bayi amesema maandalizi ya msafara wa Tanzania yamekamilika huku msafara huo utakuwa na awamu tatu  kwenda kushiriki kwenye michezo ya Olimpiki ya Paris 2024

 “Timu  hiyo itaondoka kwa makundi ambapo kundi la kwanza litaondoka litaondoka Julai 22 (mkuu wa msafara) kundi la pili Julai 23 (kuogelea)  na kundi la mwisho litaondoka Julai 27( riadha)” amesema Filbert Bayi

Tanzania katika Michezo ya Olimpiki Paris 2024 itawakilishwa na Wanamichezo 7 ambao ni Wanariadha 4,Waogeleaji  2 na mchezaji wa Judo 1.