Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Mwenda
Kamishna Mwenda amesema hayo leo Julai 15, 2024 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa TRA Makao Makuu Jijini Dar es Salaam.
Amesema mpaka sasa wamekamilisha utengenezaji wa mifumo miwili ikiwemo wa kutoa nyaraka za manunuzi na wa bei elekezi eneo la forodha na kwamba mifumo hiyo ikianza hawatarajii kupata malalamiko kutoka kwa walipakodi.
Amesema, hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwemo kusitisha kamatakamata na ufuatiliaji wa risiti za mashine za kielektoniki (EFD), kuongeza nguvu ya kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya kodi, kuweka mfumo wa utoaji nyaraka za manunuzi wakati wa uagizaji bidhaa, kubainisha na kusimamia orodha ya bidhaa nane kuwa na bei elekezi, kukamilisha maboresho ya mfumo wa Tancis na wataalamu wa forodha kukutana na Jumuiya za wafanyabiashara nchini ili kujadiliana taratibu za kiforodha.
Amesema TRA imejipanga kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa walipakodi na umma kupitia njia mbalimbali zikiwemo semina za mabadiliko ya sheria za kodi zinazogawa aina za walipakodi mfano Wauzaji wa Vitenge na wauzaji wa vito vya thamani.
"Mbali na semina Kuna Elimu ya mlango kwa mlango yenye lengo la kuelimisha na kutoa huduma kwa walipakodi wetu, kutumia mitandao ya kijamii kuelimisha, ikiwemo makundi ya WhatsApp ya wafanyabiashara kwa kutuma jumbe mbalimbali za kuelimisha kodi,kutumia matangazo ya magari na vipeperushi mbalimbali na Vikao vya wadau ikiwemo washauri wa kodi wa Kariakoo na viongozi wa wafanyabiashara kwa kujumuisha Matangazo kwenye TV, Radio, Magazeti na kutumia wasanii au watu mashuhuri jambo hili litafanikiwa.
Amesema mfumo wa kuruhusu kutoa nyaraka za manunuzi umekamilika tangu Julai 3, mwaka huu hivyo wafungashaji bidhaa (consolidator) kila mfanyabiashara atapata taarifa za kiforodha pia ataweza kulipa kodi moja kwa moja bila kupitia kwa mfungashaji na kwamba ataelewa ni kodi gani imelipwa.
Mwenda amesema maboresho ya TANCIS yakijumuisha mfumo wa Auto valuation yanaendelea na kwa sasa yapo kwenye hatua za utengenezaji wa mfumo na Maboresho hayo yatakamilika kufikia mwezi Januari, 2025 kama ilivyoelekezwa na Serikali.
Mwenda amesema kumekuwa na malalamiko kwamba kutokuwa na bei elekezi kwenye bidhaa za vitenge, mashati, nguo nyingine, vipodozi, Vito vya thamani, nguo za ndani, leso na vesti kunasababisha rushwa.
Pia amesema "Tunawafanyakazi wazuri sana wa mamlaka tutawajengea uwezo waweze kutoa huduma nzuri zaidi na wale wachache wasiowaadilifu tutachukua hatua bila kumuonea, tutawasikiliza kutafuta taarifa na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria."