Monday , 8th Jul , 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Ujenzi kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa
Barabara kwa kiwango cha lami Malagarasi – Uvinza (Kilometa 51.1) ifikapo mwezi Machi 2025 kama ilivyopangwa.

Makamu wa Rais ametoa maelekezo hayo mara baada ya kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Barabara hiyo akiwa ziarani mkoani Kigoma. Amewasihi viongozi na watendaji kuhakikisha wanasimamia kikamilifu ili barabara hiyo iweze kukamilika kwa wakati na kuwawezesha wananchi kushiriki vema shughuli za kiuchumi na ujenzi wa Taifa.

Amesema barabara hiyo ni kiungo muhimu cha uchumi na kinachowezesha kufanya biashara kwa wananchi wa Tanzania pamoja na nchi za Jirani. Amewasisitiza kuwachukulia hatua watendaji wote watakaokwamisha ujenzi wa barabara hiyo.

Makamu wa Rais amewasihi watendaji wa Wizara ya Ujenzi pamoja na Mkandarasi kutumia vema msimu huu wa kiangazi kuhakikisha wanafanya kazi kwa haraka bila kupoteza ubora unaotarajiwa ili barabara hiyo iweze kukamilika kabla ya ujio wa mvua.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Kupooza Umeme wa Msongo wa Kv 132 kilichopo Kijiji cha Nguruka Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma. Makamu wa Rais ameipongeza Wizara ya Nishati kwa maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kimefikia asilimia 95.

Amesema serikali imedhamiria kuufungua mkoa wa Kigoma ikiwemo upatikanaji wa umeme nafuu ili kuweza kuvutia zaidi wawekezaji. Ameongeza kwamba kuingizwa katika gridi ya Taifa mkoa wa Kigoma ifikapo mwishoni mwa mwezi wa tisa kama ilivyoahidiwa na Wizara ya Nishati kutawezesha wananchi kutumia fursa kujiletea maendeleo.

Pia Makamu wa Rais ameielekeza Wizara ya Nishati kufutilia mradi wa umeme wa Igamba uliyopo Wilaya ya Uvinza ili ukamilike kwa wakati na kuwezesha upatikanaji wa umeme wa kutosha katika mkoa huo.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Kigoma kufuatilia haraka na kukomesha tatizo la mifugo hususani ng’ombe kutawanywa ovyo na kula mazao ya wakulima katika Wilaya ya Uvinza. Amesema ni muhimu wafugaji kutambua matumizi bora ya ardhi kwa kutumia eneo la malisho lililotengwa na kuanza kufuga kisasa ili kuepusha migogoro katika jamii.

Aidha ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuongeza jitihada katika kulinda mazingira ikiwemo kujielekeza katika kuoanda miti na kuzuia uchomaji moto wa misitu.