Tuesday , 2nd Jul , 2024

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, George Simbachawene, amesema ujenzi wa mradi wa Mahakama ya Mwanzo ya kisasa katika Kijiji cha Kinusi unaweka historia kwani sehemu inapojengwa ni eneo gumu kufikika.

hivyo itasaidia kuchagiza utawala bora kwa wananchi wa jimbo la Kibakwe kwa ujumla. 
  
Ametoa kauli hiyo leo  katika Kijiji cha Kinusi kilichopo Kata ya Ipera,  Halmashauri ya Wilaya ya  Mpwapwa  jijni Dodoma wakati wa tukio la  kukakabidhi eneo hilo  la ujenzi wa Mahakama kwa mkandarasi.  

Amesema mradi huo wa ujenzi wa Mahakama utakaogharimu shilingi bilioni 1.1 hadi kukamilika kwake  umekuja kwa wakati  muafaka kwani wananchi hawatalazimika kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kwenda kutafuta haki zao wilayani Mpwapwa. 

Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa ujenzi wa jengo hilo unarudisha historia ya eneo hilo la Ipera kwani  miaka ya 1952 kulijengwa Mahakama na Waingereza iliyoanza kufanya kazi huku aliyekuwa  Chifu wa eneo hilo,  Chifu Zaina Sechamule  alitumika kama Hakimu.

"Kihistoria eneo hilo linajulikana  kwa jina la Kwilondoo ndiko eneo ambako kulikuwa kunapatikana haki na ndilo  eneo  alikokuwa akiishi Chifu na  huyu alikuwa ni Chifu mwanamke, hivyo leo ni siku ya kihistoria ya kukabidhi eneo la ujenzi wa mahakama ya kisasa," amesisitiza Waziri Simbachawene. 

Amesema ujio wa mahakama hiyo itasaidia kutoa haki kwa zaidi ya wananchi wa Kata sita zilizopo katika eneo hilo huku akizitaja hata  zile Kata za jirani za  Wilaya ya Kilosa, Mkoani Morogoro zitanufaika pia.