Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa (katikati) alipotembelea banda la maonyesho la GGML katika Kongamano la tatu la uzingatiaji wa ushiriki wa wazawa katika sekta ya madini lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC) Mei 2024. Kutoka kushoto kwenda kulia ni Dominic Marandu, Meneja wa Mafunzo na Maendeleo wa GGML, Rhoda Lugazia, Ofisa Mwandamizi wa Mawasiliano wa GGML, David Nzaligo, Mwanasheria mwandamizi wa GGML na Gilbert Mworia, Meneja Mwandamizi wa GGML anayeshughulia mahusiano endelevu.
Msukumo wa serikali wa kushirikisha wazawa katika mnyororo wa fursa kwenye sekta ya madini umezidi kuleta matokeo chanya kwa Watanzania kutokana na maboresho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017/2018 na marekebisho yake yaliyofuata mwaka 2019.
Mkakati huo ambao umezidi kupigiwa chapuo kupitia sheria hiyo, sasa umeifanya sekta hiyo kuwanufaisha watanzania kwani katika mauzo yote yaliyofanyika kwenye migodi mbalimbali mikubwa nchini, asilimia 90 ya mauzo yote yalifanywa na kampuni za wazawa.
Mojawapo ya kampuni ambazo zimekuwa mstari wa mbele kuzingatia kanuni hizo za kushirikisha wazawa kwenye sekta ya madini (Local content) ni Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) ambayo ni kampuni tanzu ya AngloGold Ashanti.
Kampuni hiyo pia imetajwa kuwa mfano bora wa uwajibikaji kwa jamii pamoja na kuzingatia kanuni hizo za Local content na kuboresha maisha ya watu wanaozunguka mgodi huo. Mbali na uwajibikaji wa kampuni hiyo kwa jamii, pia imezingatia kutoa kandarasi mbalimbali kwa wazawa ili kuwajengea uwezo na kuwapa uzoefu wa kupata fursa hata kwa kampuni kubwa mbali na GGML.
Katika kutekeleza malengo ya kanuni hiyo ya Local Content, zipo changamoto mbalimbali ambazo zinazikabili kampuni hizo za kizawa kushindwa kufikia vigezo vya ubora na ufanisi wa huduma zinazotakiwa kutolewa kwenye kampuni kubwa za madini kama vile GGML, hivyo katika kuwajengea uwezo wazawa, kampuni hiyo inayofanya shughuli zake za uchimbaji mkoani Geita, imewapa elimu wazawa hao kwa njia mbalimbali ikiwamo semina, warsha na madarasa malumu ambayo yamewawezesha kushinda zabuni na kutoa huduma kwa ufanisi.
Mwanasheria Mwandamizi wa GGML, David Nzaligo anasema juhudi hizo zimewezesha wafanyabiashara wazawa kufaidika na fursa zinazopatikana kwenye sekta hiyo ya madini ikiwa vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu kwa kuboresha ujuzi wao wa kuandika maandiko ya kibiashara na kushindana ipasavyo katika kuwania fursa zinazopatikana ndani ya GGML.
Kutokana na hali hiyo, idadi ya wafanyabiashara ambao ni wenyewe wa mkoa wa Geita walioingia kandarasi na GGML, imeongezeka kutoka 73 Januari 2020 hadi 96 Desemba 2023, na thamani ya biashara inayotolewa kwa wasambazaji wa Geita imeongezeka kutoka asilimia saba ya matumizi ya ndani mwaka 2020 hadi 9.4 % katika 2023.
Anasema mikakati hiyo ya GGML katika kutekelezwa matakwa ya sheria hiyo ya madini, imekuwa na faida kwa wenyeji wa mkoa wa Geita na hata nje ya mkoa huo.
“Katika robo ya kwanza ya mwaka 2024 pekee, asilimia 95 ya bajeti ya kampuni ilitengwa kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa na huduma kutoka kwa makampuni ya Tanzania. Kuongezeka huku kwa manunuzi ya ndani kumesababisha mnyororo wa thamani ya madini kwa jamii inayotunguka kuendelea kuonekana kwa kuwa sasa unastawisha na kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wao.
“Kwa mfano, GGML imeingia ubia na wafanyabiashara wa ndani ili kutoa huduma ya usafiri na usambazaji wa mafuta wenye thamani ya zaidi ya Sh 25 bilioni. Mmoja wa waza hao ni kampuni ya Blue Coast Investment Limited inayohusika na usafirishaji wa wafanyakazi ndani ya mgodi na usambazaji wa mafuta. Kampuni hii inafanya kazi za GGML pia nje Geita ikiwamo Dar es Salaam.
“Kampuni nyingine ya ndani ambayo imenufaika kutokana na GGML kutekeleza kikamilifu mikakati ya Local content ni AKO Group. Hii ni kampuni ya kitanzania ambayo imekuwa ikitoa huduma za chakula na usimamizi wa huduma zote za kihoteli ndani GGML tangu 2010,” anasema.
Anasema hatua hiyo inakwenda zaidi ya ushiriki katika shughuli za manunuzi kwani inajumuisha kubadilishana uzoefu na kuwaongezea ujuzi na teknolojia watanzania wanaoshinda zabuni hizo kupitia kampuni zao.
“Nguvukazi ya kampuni ni kipimo cha dhamira hii kwa sababu asilimia 97 ya wafanyakazi wote ni watanzania ambao pia asilimia 80 wapo kwenye timu ya uongozi wa GGML,” anasema.
Awali akizungumza katika kongamano la tatu la ushiriki wa wazawa kwenye mnyororo wa shughuli za madini lililofanyika mkoani Arusha, Nzaligo alisema "Eneo lingine ambalo GGML inatumia kunufaisha wazawa ni pamoja na uhamishaji wa teknolojia na ujuzi. Kwa Watanzania kushika nyadhifa ambazo zilikuwa zikishikiliwa na watu wasio Watanzania, huo ni msisitizo ambao umewezesha vipaji vya ndani kukua na kuwa endelevu kwa GGML,” anasema.
Kutokana na hali hiyo, GGML imeendelea kuwa mfano wa kuigwa katika kukuza na kushirikisha wenyeji katika shughuli za kiuchumi, kubadilisha maisha yao na kuchochea mabadiliko chanya katika shughuli mbalimbali ikiwamo namna ya kupata zabuni kwenye kampuni nyingine nchini.
Kutokana na mwamko huo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde anasema ana hakika kupitia mpango huo wa matumizi ya kanuni za Local Content, jumla ya trilioni 3.1 zitaendelea kubaki ndani ya nchi kupitia manunuzi na utoaji wa huduma kutoka kwa kampuni za madini kila mwaka.
Akizungumza na wajumbe wa kongamano hilo lililolenga ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini, anasema jitihada hizo zitaendelea kuwa sehemu ya mikakati ya Taifa na hata kuvutia wawekezaji wengine.
“Najua tozo zipo na zina taratibu zake, lakini kipaumbele chetu kimejikita zaidi katika eneo hili: alisema na kusisitiza kuwa manunuzi katika sekta ya madini yalifikia zaidi ya trilioni 3.1 – mwaka jana, fedha hizi zikibaki Tanzania, zitaendelea kuwa kuwa na matokeo chanya uchumi wa nchi.
Alitoa wito kwa Watanzania kutumia fursa katika sekta ya madini, kwani Sh trilioni 3.1 zinatakiwa kubakizwa ndani ya nchi.
Aliongeza katika kutekeleza mipango ya Dira ya 2030 ni pamoja na hitaji la kuhakikisha asilimia 30 ya eneo la Tanzania lifanyiwa utafiti wa kina ili kubaini madini yaliyopo.
“Kwa sasa kuna utaalamu wa kutambua maeneo yenye madini “lakini bado hatujajua wingi wake. Unapojua wingi, inakuwa rahisi kupanga.
“Hadi sasa ni asilimia 16 tu ya eneo lote lililofanyiwa utafiti, wakati upande wa Local Content umewezesha kuzalisha jumla ya ajira 18,853 mwaka 2023, ikiwa ni ongezeko la ajira 2,391 ikilinganishwa na utafiti uliopita, sawa na ongezeko la asilimia 14.5,” alisema.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa aliangazia sera ya Tanzania ya kufungua milango kwa uwekezaji katika madini, akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na wadau ili kutimiza mikakati ya Dira ya 2030 ambayo inalandana na kauli mbiu isemayo "Madini ni Maisha na Utajiri."
Naibu Waziri huyo aliwahakikisha wdau hao wa sekta ya madini kuwa serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia uwekezaji zaidi hasa katika sekta ya viwanda vya malidhafi za madini.