Thursday , 6th Jun , 2024

Wasimamizi na wadau wa afya mkoani Morogoro, wameaswa kushirikiana kwa ukaribu na Bohari ya Dawa (MSD), ili kwa pamoja waweze kutatua na kuboresha hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya mkoani humo, kwa ajili ya ustawi wa watu na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Rai hiyo imetolewa hapo na Kaimu Mkuu wa Mkoa wà Morogoro, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini Mhe. Rebeka Nsemwa, wakati akifungua kikao kazi cha wateja na wadau wa MSD Kanda ya Dar es Salaam, kilichokutanisha viongozi wa sekta ya afya ngazi ya mkoa na wilaya mkoani humo.

"Mkoa huu una jumla vya vituo 378 vya kutolea huduma za afya ambavyo vinajumuisha hospitali kumi na sita(16), ikiwemo hospitali mbili za rufaa, vituo vya afya arobaini na sita (46) na zahanati mia tatu kumi na sita (316), hivyo fanyeni kazi kwa pamoja na kujadiliana namna bora ya kuboresha utekelezaji wa majukumu yenu, na hata kupeana mrejesho wa masuala mbalimbali yanayohusiana na mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya.” Alisisitiza Mhe. Nsena

Mhe. Nsemwa amewataka viongozi hao kuhakikisha wanakuwa na majadiliano yenye tija kwa kuainisha namna bora ya kufanya kazi kwa pamoja, badala ya kutupiana lawama na kunyosheana vidole, ili kila upande uweze kutimiza wajibu wake katika kuwahudumia wananchi.