Thursday , 23rd May , 2024

Wananchi wa Kata ya Mgwashi katika jimbo la Bumbuli wilayani Lushoto Mkoani Tanga wamelalamikia kuchelewa kwa mradi wa kituo cha afya ambacho kilianza ujenzi mwaka 2022 huku wanaopata shida kubwa ni wakinamama wajawazito ambao wanakosa mahali pa kujifungulia.

Serikali ilitoa shilingi milioni 500 kwajili ya jengo hilo na lilipaswa kufunguliwa mwezi septemba mwaka 2022 sawa na miaka miwili iliyopita lakini mpaka sasa bado ujenzi wake unaendelea. 

Wakizungumza na EATV saa moja baadhi ya wananchi hao wamesema wapo hatarini kupoteza maisha yao kutokana na changamoto ya kucheleweshwa kukamilika kwa majengo matano kituoni hapo kwani baadhi ya huduma wamekuwa wakizikosa jambo linalowalazimu kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo. 

"Sisi wakina mama tunanyanyasika unakuta mtu ni mjamzito hana elfu hamsini ya kuweka gari mafuta kwenda Lushoto mjini au Bumbuli unakuta mtu kashafikia kujifungua hela huna mpaka uende ukakope pesa ya mafuta huku mtu anahangaika na wengine wanapoteza maisha, "alisema mmoja wa mama. 

Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Japhar Kubecha amesema hatua za awali zimekwisha kufanyika za kuhakikisha waliohusika kuhujumu mradi huo zinachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwaondoa kazini watumishi waliohusika na mchakato wa manunuzi. 

"Hatua nyingine za ndani zinaendelea ikiwemo mzabuni aliyeshiriki kwenye jambo hilo hili jambo tunalifanyia kazi n tayari tumeshaweka makubaliano na Mkurugenzi ndani ya hizi wiki mbili mpaka tarehe moja mwezi wa sita majengo haya yawe yameshaanza kufanya kazi, "alisema Kubecha. 

Akizungumza na wananchi wa Mgwashi Mjumbe wa Halmashauri ya CCM Taifa Mohamed Ratco amehoji sababu za mradi huo kutokamilika kwa wakati licha ya kwamba mradi huo umeanza muda mrefu huku wananchi wakiendelea kukabiliana na changamoto ya huduma hiyo. 

Aidha mara baada ya kubainika moja ya sababu iliyochelewesha mradi huo ni kutokana na uzembe uliofanyika wa MNEC Ratco alimtaka mtu wa manunuzi aliyezidishiwa fedha kiasi cha shilingi milioni 36 kwa uzembe  achukuliwe hatua ili azirejeshe fedha hizo na kituo hicho kiweze kukamilika kwa wakati na wananchi waweze kupata huduma. 

"Tunapaswa kuwa makini sana huu ni uzembe umefanyika na aliyehusika kwenye uzembe hui lazima ajulikane na hata kama kuma sehemu kahamishwa ni lazima sheria ichukue mkondo wake hatuwezi kuacha ubovu hapa halafu mtu apelekwe sehemu nyingine ndani ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania hili halikubaliki niombe huu uzembe ujulikane nani amesababisha tusiishie tu kusema kwamba kulikuwa na kamati, "alisema.