Thursday , 22nd Feb , 2024

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje Balozi Shaibu Mussa, amesema kwa mtu yeyote ambaye ana mashaka na uhalisia wa taswira ya sanamu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere iliyojengwa kwenye ofisi za Makao Makuu ya AU, Addis Ababa nchini Ethiopia aulizwe mtoto wake Madaraka.

Taswira ya Sanamu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyowekwa kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU), Addis Ababa

Kauli hiyo ameitoa hii leo Februari 22, 2024, wakati akizungumza mbele ya wahariri na waandishi wa habari Ikulu ya Dar es Salaam, baada ya kuibuka kwa maoni mchanganyiko kutoka kwa Watanzania ambao wengi wao walisema sanamu hiyo haifanani na Baba wa Taifa, ambapo serikali pamoja na familia ilijiridhisha kuhusu taswira ya sanamu hiyo.

"Kamati ya kutengeneza sanamu ilihusisha wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilihusisha familia ya Mwalimu Nyerere akiwemo Madaraka Nyerere ilihusisha watu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, watu kutoka Wizara ya Utamaduni ambao waliunda jopo la wataalamu na watu wengine wa masuala ya kutengeneza sanamu, kamati iliridhika kwa sababu mwalimu mnayemuona katika sanamu lile la Addis ni mwalimu anayeeelezwa wa miaka ya 60 hadi 80 wakati yuko active katika mapambano ya kusaidia kuleta uhuru na maendelea Kusini mwa SADC," amesema Balozi Shaibu

Aidha ameongeza kuwa "Lakini pia kauli ya mwanae Madaraka Nyerere ameitoa mara kadhaa na mpaka siku ya uzinduzi mimi nilikuwepo Madaraka aliendelea kusisitizxa kwamba yule ni Baba yake na akama kuna mtu ambaye anabisha basi amuulize yeye,".