Thursday , 15th Feb , 2024

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewaagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kutafuta ufumbuzi kuhusu suala la kuharibika kwa barabara kabla ya muda uliopangwa ili kuokoa fedha za Serikali zitakazotumika kurekebisha miundombinu hiyo.

Agizo hilo amelitoa jijini Dodoma Februari 14, 2024 katika kikao cha 19 cha Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS na kuwasisitiza kusimamia miradi kwa weledi na uzalendo ili kusaidia miradi kukamilika kwa viwango na kwa wakati.

Aidha, Bashungwa ameagiza TANROADS kutumia kikamilifu mtambo wa Ukaguzi wa Barabara (Road Scanner) wakati wa kufanya ukaguzi wa miradi ya barabara na madaraja na hata kutumia vifaa vingine vitakavyoweza kuwasaidia kubaini ubora wa mradi mapema kabla ya kukabidhiwa. 

Ameielekeza TANROADS kuimarisha na kukijengea uwezo Kitengo chake cha Usimamizi wa miradi (TECU), ili kusimamia miradi kwa weledi na ufanisi.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohamed Besta, amemhakikishia Waziri Bashungwa kutekeleza maagizo aliyowapa na kuendelea kufanya kazi kwa ari na bidi katika utendaji wao wa kila siku ili kuleta tija kwa Wakala huo.

Naye, Mweyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati, Ujenzi na kazi nyingine (TAMICO), Eng. Nchama Wambura, amesema wataendelea kushrikiana na  kufanya kazi kwa bidii ili kuleta mabadiliko chanya na maendeleo kwa utekelezaji sahihi na ubora kwa miradi wanayoendelea kutekeleza nchini.

Mkutano wa 19 wa Baraza la wafanyakazi la TANROADS, umefanyika Dodoma kwa siku 2 na kushirikisha zaidi ya wajumbe 100 kutoka Mikoa yote nchini.