Wednesday , 7th Feb , 2024

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema Serikali itahakikisha inaendelea kutumia teknolojia ya kisasa kwa kadri inavyowezekana kudhibiti wanyama wakali na waharibifu hususan tembo ili kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyamapori.

Ameyasema hayo leo Februari 7, 2024 katika kikao chake na Wabunge wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kilicholenga kusikiliza changamoto  wanazokabiliana nazo wananchi katika  kuthibiti  wanyamapori wakali  na waharibifu katika maeneo yao kilichofanyika leo jijini Dodoma. 

“Katika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo tunatumia teknolojia ya Geofencing ambapo tutaweza kupata taarifa endapo tembo  amesogea karibu na uzio uliowekwa na hivyo askari wetu watachukua hatua  za haraka” Mhe. Kairuki amefafanua.

Kuhusu uzio wa umeme amesema Serikali inaendelea na majaribio kuona kama njia hiyo inafaa au la ambapo kwa sasa majaribio yamefanyika Pori la Akiba la Grumet.

Amesema pia Serikali inafanyia kazi madai ya kifuta jasho na kifuta machozi ambapo mpaka sasa uhakiki umeshafanyika hivyo ufuatiliaji wa fedha unaendelea ili wahusika walipwe.

Kuhusu kutangaza vivutio vya utalii vya ukanda wa kusini, Mhe. Kairuki amesema Serikali itafanya tathmini ya kina kuweza kuviibua, kuvitangaza na kuviendeleza  vivutio vya utalii vya Ukanda wa Kusini hasa Kilwa Kisiwani na maeneo ya fukwe ya Pangani, Mkinga na Mafia.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mhe. Salma Kikwete amesema maeneo mengi ya Mikoa ya Lindi na Mtwara yanakabiliwa na changamoto ya tembo hivyo kuiomba Serikali kutafuta ufumbuzi wa muda mrefu ili kuepuka madhara yanayowapata wananchi hasa kuliwa mazao yao.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb)  Wabunge wa Mikoa ya Lindi na Mtwara, Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake za Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA)  na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS)