Friday , 26th Jan , 2024

Walimu wa shule ya msingi Nyansalala iliyopo kata ya Bukondo Halmashauri ya wilaya ya Geita, wamelazimika kufanya kazi wakiwa wamekaa chini baada ya kamati ya shule na uongozi wa kijiji hicho kuwanyang’anya madawati waliyokuwa wakiyatumia ofisini kama mbadala wa viti na meza.

Walimu wakiwa wamekaaa juu ya madaftari

Akielezea tukio hilo mwalimu mkuu wa shule hiyo Mwalimu Joseph Mfungi amesema alipigiwa simu na  Mwalimu Mkuu Msaidizi kuwa Afisa Mtendaji wa kijiji hicho amewataka walimu kuwapatia wanafunzi madawati waliyokuwa wanakalia kwani madawati hayo yameletwa kwa ajili ya wanafunzi.

"Niliamua kuahirisha safari nikaja haraka haraka shuleni baada ya kupata taarifa hiyo, nilikuta walimu wamekaa chini wamekata tamaa kila mmoja anahuzunika kivyake wapo wamekaa kwenye viunga vya shule, nikauliza shida nini wakasema ofisini hakuna viti vya kukalia na yale madawati mtendaji kayapeleka darasani kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi," amesema Mwalimu Mkuu.

Chama cha Walimu wilaya ya Geita walifika katika shule hiyo na kujionea changamoto wanayoipitia walimu wa shule hiyo huku wakilaani kitendo kilichofanywa na uongozi wa kijiji hicho.