Monday , 22nd Jan , 2024

Mkuu wa Wilaya ya Hanang Janeth Mayanja amesema Serikali itaendelea kushirikana na Taasisi pamoja na Mashirika mbalimbali ya kijamii katika kuimarisha na kutoa huduma kwa wananchi na kuirudisha Hanang katika hali yake ya awali kama ilivyokuwa kabla ya kutokea maporomoko ya Mlima Hanang.

DC Mayanja amebainisha  hayo wakati akizungumza na mamia ya wanafunzi wa shule 8 za msingi ambao walikuwa wakipatiwa msaada wa kisaikolojia kwa njia ya michezo ili warejeshe afya zao za akili katika hali ya kawaida kufuatia mafuriko ya tope yaliyoikumba Hanang mwishoni mwa mwaka 2024.

"Kama tunavyojua michezo ni burudani, michezo huleta watu pamoja, huleta mshikamano lakini pia michezo inaimarisha afya za akili, na toka tukio la mafuriko limetokea kila mmoja ambaye ameshuhudia tukio lile kwa ukubwa wake kimsingi afya yake ya akili haijakaa sawa lakini wako wataalamu wa saikolojia wanaendelea kupita nyumba kwa nyumba ili kuwarejesha wananchi wa Hanang katika hali zao za kawaida" alisema DC Janeth Mayanja

Aidha katika hatua nyingine DC Janeth Mayanja amewataka wakazi wa Hanang kucha kunung'unika na kuendea kumshukuru Mungu kwa kila jambo kwa kipindi hiki ambacho wanaendelea kurejea katika hali zao za kawaida kama ilivyokuwa awali kabla ya kutokea kwa mafuriko ya tope Desemba 03, 2023. 

Awali akizungumza wakati wa kufunga mashindano ya mpira wa miguu yaliyoandaliwa na Save The Children na kisha kushirikisha Shule nane (8) za msingi zilizoathiriwa na Mafuriko Wilayani Hanang Mkoani Manyara Abdulmajid Faraj akimwakilisha Mkurugenzi Save The Children alisema lengo la mashindano hayo ni kuwarejesha wanafunzi katika hali zao za kawaida baada ya janga la maporomoko ya tope kutoka Mlima Hanang.

“Wakati Shule zimefunguliwa mahudhurio yalikuwa madogo tukaona tutumie michezo kama chachu ya kuboresha yale mahudhurio ya watoto shuleni, lakini wakati huohuo tuweze kutumia michezo kama njia bora ya kuponyesha yale majeraha ya kisaikolojia ya Afya ya Akili” alisema Abdulmajid Faraj

Baadhi ya Wanafunzi walioshiriki katika michezo hiyo walisema imewasaidia kuamsha Ari ya kujifunza na kuwarejesha katika hali ya Kawaida licha ya athari za kisaikolojia walizozipata.