Thursday , 4th Jan , 2024

Mwanamke aitwaye Bugumba Misalaba mkazi wa Kijiji cha Nyakato, Kata ya Nyanguku Halmashauri ya mji wa Geita anayedaiwa alifariki miaka mitatu iliyopita ameonekana akiwa hai kijijini hapo jambo ambalo limesababisha mshangao mkubwa miongoni mwa wananchi wa eneo hilo.

Mwanamke anayedaiwa kufariki miaka mitatu iliyopita

Wakizungumza ndugu mwanamke huyo wamesema ndugu yao alifariki September 15, 2020 kwa ajali baada ya kugongwa na gari akiwa kwenye baiskeli akitoka Sengerema mkoani Mwanza kumtembelea baba yake mdogo na kupelekea kifo chake palepale.

"Ni kweli dada yetu huyu Bugumba Misalaba alifariki mwaka 2020 kwa ajali eneo la Igaka  na kusababisha kifo chake hapohapo ni kweli tulipata taarifa tukaenda tukakuta amefariki kweli tukamsafirisha mpaka nyumbani, tukafanya mazishi toka 2020 mpaka tarehe 1 ya mwaka huu 2024 ndiyo tukapata taarifa kuwa ndugu yetu amepatikana hapa senta tulipofika tukakuta kweli ni yeye" amesema mmoja wa ndugu yake.

Mkuu wa wilaya ya Geita Cornel Magembe, alifika eneo la tukio akiambata na kamati ya ulinzi na usalama na kuwataka wananchi wa eneo hilo kuacha tabia zenye viashiria vya imani za kishirikina.