Monday , 1st Jan , 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa watanzania kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na waumini mara baada ya kushiriki Ibada ya Mwaka Mpya katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege Dodoma.

Amesema ni muhimu Watanzania kuendelea kukemea na kupinga utengano, udini ukabila pamoja na siasa za chuki, ambapo pia amewasihi watanzania kufanya kazi kwa bidii, maarifa na nidhamu ili kuinua maisha ya familia, jamii na taifa kwa ujumla.

Makamu wa Rais amewataka watumishi wa umma na viongozi wa umma kutimiza wajibu wao ipasavyo wa kuwahudumia wananchi kwa kufanya kazi kwa uadilifu na kutenda haki wakati wote wanapotoa huduma na kuwasihi kufanya kazi kwa hofu ya Mungu na kuachana na tabia za kuwapa kesi wananchi wasiohusika na kesi hizo.

Ameongeza kwamba kwa mwaka 2024 serikali itaendelea kuimarisha demokrasia, utawala wa sheria, haki, amani na umoja, sambamba na kuwasihi wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kuanza shule kwa mwaka huu 2024 wanaanza masomo yao na wakati wote kufuatilia maendeleo ya watoto hao shuleni.