Wednesday , 13th Dec , 2023

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, amesema upo umuhimu wa kuongeza juhudi za kisera juu ya matumizi ya bidhaa za mkonge ili kudhibiti matumizi ya bidhaa za plastiki ambazo zinatokana na mazao yanayoweza kuzalishwa hapa nchini. 

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe,

Waziri Bashe ameyasema hayo wakati wa mkutano wa Nne wa Wadau wa Sekta ya Mkonge Tanzania (TSB) uliofanyika wilayani Korogwe mkoani Tanga uliokwenda sambamba na uzinduzi wa mfuko wa WAKFU,  mfuko unaolenga kufanya maendeleo ya zao la mkonge nchini. 

Waziri Bashe amesema matumizi ya bidhaa zinazotokana na zao la mkonge ndani ya nchi yameshuka huku akilinganisha na msimu wa mwaka 2019 mauzo yalifikia dola milioni 7 ambapo kwa sasa mauzo yameshuka hadi kufikia dola milioni 4.3.

Kufuatia hatua hiyo Waziri Bashe ameahidi kufanya mazungumzo na Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na Waziri wa Mazingira ili kuweka mikakati ya kanuni za kuzuia matumizi ya bidhaa za plastiki kwenye mazao ambayo yanazalishwa na kutumia bidhaa za ndani. 

"Tunapozungumzia bidhaa ni pamoja na kamba zinazotokana na mkonge lakini sasa bidhaa zake kwa matumizi ya ndani zimeshuka mpaka dola milioni 4.3 hivyo kuna umuhimu wa kuongeza juhudi za kisera juu ya matumizi ya bidhaa za mkonge na mimi hili nalipokea, tutarudi kwenda kujadiliana na mawaziri wenzangu, juu ya kanuni zinazodhibiti matumizi ya plastiki kwenye mazao ambayo tunaweza kuzalisha na kutumia vitu ambavyo tunazalisha ndani,"alisisitiza Bashe.