Tuesday , 14th Nov , 2023

Imeelezwa kuwa kundi la vijana nchini wenye umri wa kati ya miaka 15 mpaka 24 wanaongoza kwa kuchangia maambikizi mapya ya VVU na UKIMWI ambayo ni sawa na asilimia 40 (40%).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama ameyasema hayo mapema leo Ofisini kwake Jijini Dodoma ikiwa ni maandalizi ya kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani, yanayofanyika Desemba Mosi kila mwaka.

Akiongelea kuhusu maadhimisho hayo yanayotarajiwa kafanyika kitaifa mkoani Morogoro, Waziri Mhagama amesema tafiti zilizopo zinaonesha kuwa kuna kila sababu ya kuongeza nguvu kubwa kwa kundi la vijana ili kuliondoa kwenye uhatarishi wa maambukizi ya vvu.

Aliendelea kusema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yatatoa kipaombele kwa kiasi cha cha kutosha kwa vijana kushiriki kikamilifu kwenye majukwaa na matukio yaliyoandaliwa kwenye maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani mwaka huu nchini kote kutokana na sababu kwamba vijana ndo waingia kwenye maambukizi mapya kwa wingi.

"Tunapokwenda huko mbele walau kwenye maadhimisho ya wiki ya kuelekea siku ya UKIMWI Duniani, tutoe nafasi ya kuwasikiliza vijana kwa karibu zaidi wakongamane, wakutane na viongozi wa dini na viongozi wa kimila, na wakati mwingine tumekuwa tukifikiri kwamba labda, mienendo ya kimaadili kwa sasa imekuwa ikichagiza vijana wetu kujikuta wanaingia kwenye kundi la maambukizi mapya kwa hivyo kwa kipindi hiki kipaombele kitakuwa kwa kundi la vijana," amefafanua Waziri Mhagama.

Aidha, Waziri Mhagama amesema kuwa zaidi ya mara tano tafiti zinaonesha kuwa wanawake wamekuwa na uhiyari wa kupima ukilinganisha na wanaume; ambao hawajitokezi kupima na kuanza matumizi ya dawa, hivyo kuna kila haja ya Serikali kupaza sauti juu kuwaomba kina baba waingiwe na hali ya uhiyari katika kufanya maamuzi ya kupima.