
Mtuhumiwa Andrea ametiwa nguvuni kufuatia agizo la Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera kwa vyombo vya ulinzi na usalama kumsaka mtuhumiwa baada ya kufika eneo la msitu wa hifadhi ya pori la akiba na Rungwa South likiwa limefyekwa na kuelezwa kuwa eneo hilo limeuzwa kwa mmoja wa wananchi kutoka Mkoani Tabora.
Homera amesema kuwa mtuhumiwa amekuwa na utaratibu wa kutafuta watu na kwenda nao katika msitu huo na kuwauzia baadhi ya maeneo kwa kuwakatia kila mteja kipande cha ardhi kwa kuanzia ekari 200 –400 kwa ajili ya kilimo na mifugo.
‘Hivi ninavyozungumza mtuhumiwa amekamatwa na yupo ndani kituo cha Polisi Mbeya ili azidi kuwataja na wenzake waliokuwa wanafanya hiyo kazi ya kuuza pori sehemu ya Rungwa South ambacho ni kitalu kikubwa cha uwindaji na kimekuwa kinaiingizia mapato Serikali na fedha za kigeni’ amesema Homera, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Mtuhumiwa yupo kituo cha Polisi na baada ya taratibu zote kukamilika atafikishwa mahakamani muda wowote kwa kosa na kuuza Sehemu ya Msitu wa Pori la akiba na Msitu wa Rungwa South.