Saturday , 28th Feb , 2015

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa amewataka wananchi kutosikiliza maneno yanayosemwa mitaani kuhusiana na katiba inayopendekezwa na badala yake waisome katiba hiyo vizuri na kuielewa ili waweze kufanya uamuzi wao siku ya kuipigia kura.

Gallawa ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kufuatia mkoa huo kupata jumla ya nakala 61,290 za katiba inayopendekezwa ambazo zimeanza kusambazwa kwa wananchi.

Alisema kuna baadhi ya watu na wanasiasa ambao wanapita na kuwataka wananchi kutoipigia kura katiba inayopendekezwa hata kabla ya wananchi hao hawajaisoma na kujua ni kitu gani kilichoandikwa humo ndani.

Amewataka Watanzania kujiridhisha kwa kuisoma kwa makini kabla ya kuipigia kura ya ndiyo au hapana kwani ni haki yao ya kikatiba.

“Kususa kupiga kura siyo suluhisho kwani usipopiga kura utakuwa hujaitumia haki yako ya kikatiba ipasavyo,” alisema Chiku Gallawa na kuongeza,

“Watanzania ni lazima wabadilike kwani siyo kila kitu wanachoambiwa wakubaliane nacho ni lazima wajiulize huyo anayewakataza kupiga kura ana maslahi gani na hiyo katiba?”

Amewataka wananchi waisome kwa makini katiba hiyo na kuielewa ili siku ya kuipigia kura wawe na maamuzi sahihi ya kuipigia kura ya ndiyo au hapana kuliko kusikiliza maneno ya watu wanaowaambia kuwa katiba hiyo haifai.

Hivi karibuni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, John Mnyika aliwakataza wanawake wa chama hicho kuipigia kura katiba inayopendekezwa wakati akizungumza nao kwenye mkutano mkuu wa baraza la wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) uliofanyika kwenye ukumbi wa African Dreamz Mjini Dodoma.