Friday , 27th Feb , 2015

Imeelezwa kuwa uelewa mdogo wa wananchi kuhusiana na kazi za kikosi cha zima moto ndiyo changamoto kubwa inayokikabili kikosi hicho mkoani Dodoma.

Kikosi cha Zima moto kikiwa katika harakati za kuuzima moto

Hayo yameelezwa leo na Mkuu wa kikosi cha Zimamoto Mkoani Dodoma, Yohana Nkunu wakati akizungumza kwenye hafla ya kufunga mafunzo ya askari wa zimamoto yaliyofanyika katika ofisi za zimamoto mkoa wa Dodoma.

Nkunu amesema kama jamii ingekuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na kazi za zimamoto kazi ya kukabiliana na majanga ya moto pamoja na uokozi ingekuwa rahisi kwani wananchi wenyewe ndiyo kikwazo katika kutekeleza majukumu ya jeshi hilo.

Kwa upande wake luteni Jumanne Maganga kutoka kambi ya Jeshi la wananchi (JWTZ) kambi ya Ihumwa amesema kuwa jeshi hilo limeamua kupata mafunzo ya kuzima moto ili liweze kusaidia kuzima majanga ya moto katika maeneo yanayowazunguka.

Amesema kwa muda mrefu jeshi hilo halikuwa na vifaa vya kuzimia moto na ndiyo maana walikuwa hawawezi kukabiliana na majanga hayo lakini kwa sasa watashirikiana kwa ukaribu ili waweze kuokoa maisha ya wananchi yanayofupishwa na moto.