Wednesday , 18th Oct , 2023

Huku karibu kura zote zikiwa zimehesabiwa katika uchaguzi wa Liberia, Rais George Weah na mpinzani wake mkuu Joseph Boakai bado wanachuana vikali , ikimaanisha kuwa wamejipanga kwa duru ya pili.

Bw Weah kwa sasa ana asilimia 43.8 ya kura huku Bw Boakai akiwa na asilimia 43.5, matokeo ya awali yanaonesha.Mgombea anahitaji zaidi ya asilimia 50 ya kura kutangazwa mshindi.

Uchaguzi wa Oktoba 10 ulikuwa wa msisimko  zaidi nchini Liberia tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe miongo miwili iliyopita.

Tume ya uchaguzi ilitoa matokeo   baada ya kura kuhesabiwa katika zaidi ya asilimia 98 ya vituo vya kupigia kura na kumpa Bw Weah ushindi mwembamba wa kura 5,456.

Upigaji kura unatarajiwa kurudiwa katika baadhi ya maeneo ya kaunti za Sinoe, Nimba na Montserrado siku ya Ijumaa baada ya kura kupigwa na watu wasiojulikana, tume hiyo imesema.