Tuesday , 26th Sep , 2023

Chama cha wachezaji wa kulipwa England PFA, kimeomba kuingilia kati na kusaidia kutatua mgogoro unaoendelea kati ya kocha wa Manchester United Eric ten Hag na winga wa timu hiyo Jadon Sancho. Sancho amefungiwa kutoshiriki kwenye shughuli zote za kikosi cha kwanza cha Man United.

Kushoto ni winga wa Manchester United Jadon Sancho na kulia ni kocha Erik ten Hag

Chama cha wachezaji wa kulipwa England PFA kinatajwa kiliomba kusaidia kutatua hali ya kutokwa na maelewano kati ya kocha wa Manchester United Erik ten hag na mchezaji wake Jadon Sancho. Kwa sasa Sancho ameondolewa kwenye kikosi cha kwanza cha the Red Devils baada ya kupishana na Ten hag.

Sancho aliingia kwenye mgogoro na kocha Ten hag baada ya mchezaji huyo kukanusha na kusema taarifa ya kocha wake kuwa ni ya uongo kupitia mitandao ya kijamii. Sancho alikanusha taarifa hiyo baada ya kocha huyo kusema kuwa Sancho hakufanya vizuri mazoezini ndio maana hakuwa sehemu ya mchezo wa Ligi kuu dhidi ya Arsenal.

Jana Jumatatu iliripotiwa kuwa Sancho kwa sasa amefungiwa kutoshiriki kwenye mazoezi yote ya kikosi cha kwanza cha Manchester United ikiwemo matumizo ya vifaa, uwanja wa mazoezi na hata sehemu ya chakula. Sancho anakumbana na adhabu hii ikiwa ni sehemu ya adhabu ya utovu wa nidhamu dhidi ya kocha wake, na inatajwa kuwa mchezaji huyo amegoma kuomba radhi.