
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Kanali Boniphace Maghembe (wa pili kushoto) akipokea nyaraka za vifaa mbalimbali vya tiba kutoka kwa Ofisa Mwandamizi Mahusiano ya Jamii kutoka GGML, Musa Shunashu (wa kwanza kulia).
Msaada huo wenye thamani ya Sh260 milioni, unajumuisha vitanda 17 vya hospitali, vitanda vitano vya uchunguzi wa kitabibu, majokofu maalumu ya kukusanya damu na magodoro.
Pia imetoa vifaa maalumu vya uchunguzi wa via vya uzazi kwa mwanamke, viua wadudu, majokofu ya kuhifadhia maiti, vifaa vya upasuaji, mashine za kufulia na darubini.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo jana mkoani Geita, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Kanali Boniphace Maghembe aliishukuru GGML kwa ukarimu wao kwa jamii inayozunguka migodi.
"Ni furaha yangu kutambua kuwa tangu GGML ianze kazi hapa Geita, wameshirikiana kwa karibu na Serikali kutekeleza miradi kadhaa ya afya hususan ujenzi wa zahanati na vituo vya afya," alisema
Aidha, Meneja Mwandamizi anayesimamia mahusiano endelevu ya kijamii kutoka GGML, Gilbert Mworia, alisisitiza umuhimu wa huduma bora za afya katika kufikia lengo la 3 la Umoja wa Mataifa la Maendeleo Endelevu, ambalo linalenga katika kuhakikisha maisha ya afya na kukuza ustawi kwa wote.