Thursday , 14th Sep , 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amewataka Majaji wa Mahakama Kuu na wale wa Mahakama ya Rufani, kuhakikisha wanasimamia haki za watu na sio kupindisha haki ya mtu kwa pesa kidogo ambazo mwisho wa siku hazitowasaidia popote.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Kauli hiyo ameitoa hii leo jijini Dar es Salaam, mara baada ya kuwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni, wakiwemo majaji hao pamoja na Naibu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

"Hakikisheni mnasimamia haki za watu, mwenye haki aipate, unajua suala la kutoa haki ni la Mungu peke yake, sasa kama Mungu amekujaalia umeteuliwa kusimamia haki za wanadamu wenzio unafanya kazi inayofanana hapo, kasimamieni haki sababu mmeapa na mmeshika vitabu mnavyoviamini, mtakwenda kuulizwa kwanini ulipindisha haki kwa pesa chache ambayo ukitumia hata mwezi haufiki, hata kama utajenga lijumba la fahari halafu si utakufa utaliacha, na ukiliacha watoto wako wanauza," amesema Rais Samia  

Aidha akizungumzia suala la serikali kuingia mikataba mbalimbali ya uwekezaji na mataifa mengine, amemtaka Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Balozi Profesa Kennedy Gastorn, akawe mstari wa mbele kuhakikisha serikali haiingii kwenye matatizo ya kiuwekezaji.

 Awali akizungumza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewapongeza walioapa hii leo kwa kupata nafasi ya kuaminiwa na Rais Samia huku matarajio yake  ni kuona utendaji wenye weledi, uaminifu na uadilifu wa dhati.