Monday , 4th Sep , 2023

Mkuu wa jeshi nchini Gabon, Jenerali Brice Oligui Nguema, ameapishwa kuwa rais wa mpito wa nchi hiyo kiapo kilichofanyika katika mji mkuu Libreville.

Jenerali Brice Oligui Nguema ameapishwa hii leo kuwa rais wa mpito wa Gabon

Jeshi lilimng'oa madarakani rais Ali Bongo siku ya Jumatano muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi uliokumbwa na utata.

 

Akizungumza baada ya kuapishwa kuwa rais wa mpito wa Gabon, Jenerali Brice Nguema alitetea kutwaliwa kwa madaraka wiki iliyopita, akisema kuwa ni kitendo cha kizalendo.

Alimnukuu kiongozi wa zamani wa jeshi la Ghana, na baadaye rais aliyechaguliwa Jerry John Rawlings, akisema: "Wakati watu wanavunjwa na viongozi, basi ni jeshi ambalo lazima liwape heshima na uhuru wao.

"Ni katika roho hii kwamba sisi vikosi vya ulinzi tulichukua majukumu yao kwa kukataa... mchakato wa uchaguzi." Mwisho wa kumnukuu

 

Wafuasi wa uongozi wa kijeshi nchini Gabon wamehudhuria kuapishwa kwa Jenerali Nguema.Hali ya utulivu nchini humo ilikua  shwari lakini kwa usalama ulioimarishwa.Kiongozi huyo wa mapinduzi anasemekana kuwa binamu wa rais aliyepinduliwa Ali Bongo, na kuibua mashaka iwapo kweli hii inaashiria kumalizika kwa enzi ya Bongo iliyodumu kwa miaka 55.

Jenerali Nguema amesema hatakimbilia kuirejesha nchi hiyo katika utawala wa kiraia, ili kuepuka makosa yaliyopita.Upinzani umeonya kuwa jeshi halionyeshi ishara yoyote ya kukabidhi madaraka.

Gabon ni nchi ya sita ya Ufaransa kuanguka chini ya utawala wa kijeshi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita wakati taifa hilo la zamani la kikoloni Ufaransa likipambana kudumisha ushawishi wake barani humo.