Friday , 1st Sep , 2023

Muungano wa upinzani nchini Gabon umelishutumu jeshi kwa kutoonyesha dalili zozote kwamba baada ya kumpindua rais wa zamani Ali Bongo wanapanga kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia. 

Msemaji wa muungano huo, Alexandra Pangha, ameiambia BBC kuwa itakuwa ni upuuzi kwa wababe hao kumuapisha rais siku ya Jumatatu kabla ya kuondoa utawala wa kijeshi.

Alikosoa kusita kwao kufanya mazungumzo na chama alichosema kilishinda uchaguzi wa rais wa Jumamosi iliyopita.

 Bi Pangha amesema na kuongeza kuwa hakuamini kwamba kinasaba cha Bongo kimeondoka madarakani, na kwamba upinzani umekuwa ukisubiri mwaliko kutoka kwa jeshi ili waweze kuzungumza kuhusu mipango yao.

Alidai, bila kutoa ushahidi, kwamba kiongozi wa mapinduzi, Jenerali Brice Oligui Nguema, alikuwa akiungwa mkono na wanafamilia wengine.

Wakati huo huo Umoja wa Afrika umesitisha ushiriki wa Gabon katika shughuli zake zote kufuatia hatua ya jeshi la nchi hiyo kuchukua madaraka Jumatano, hatua ambayo imeilaani vikali.

Uamuzi huo umefuatia mkutano uliofanyika siku ya Alhamisi wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja huo.

Mapema, serikali ya Gabon ilisema itaingia katika kile inachokiita taasisi za mpito baada ya kuondolewa kwa Rais Ali Bongo.

Wanajeshi hao hawakutoa maelezo ya kina kuhusu muda gani watasalia katika eneo hilo wala kwa namna gani au iwapo madaraka yanaweza kurejeshwa kwa serikali ya kiraia.