Thursday , 31st Aug , 2023

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba mwaka 2023,

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama

Baada ya Mamlaka ya hali hewa nchini (TMA) kutoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu wa vuli zinazotegemewa kuanza katika kipindi hicho, ambao umeonesha uwepo wa El-Nino itakayosababisha vipindi vya mvua kubwa.

Waziri Mhagama amesema kipindi hicho cha mvua kubwa kinaweza kuendelea mpaka mwezi Januari 2024, na kusema msimu wa mvua za vuli ni mahususi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka unaohusisha maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Kusini mwa mkoa wa Simiyu, Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia) na Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro.

"Tunaona madhara kadhaa yanayoweza kutokea katika baaadhi ya sekta kutokana na uwepo huo wa El-Nino utakaosababishwa na mvua kubwa katika kipindi hicho ambacho kimesemwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini ni kama vile, mafuriko yatakayoleta uharibifu wa miundombinu, madhara ya kiafya, kiuchumi, kijamii na upotevu wa mali na maporomoko ya ardhi kuathiri makazi," Alifafanua Waziri Mhagama

Aidha, ameongeza kusema kuwa madhara mengine yanaweza kutokea katika sekta ya mazingira ikiwa ni pamoja na uharibifu wa  mashamba, miundombinu ya usafiri na shughuli zingine hususani uchimbaji madini pamoja na magonjwa ya milipuko kwa binadamu, wanyama na kuongezeka kwa wadudu waharibifu wa mazao na mimea.

Sambamba na hilo, Waziri Mhagama amesema serikali inaelekeza kamati za usimamizi wa maafa na sekta, kushirikiana na umma kuchukua baadhi ya hatua kama vile kutambua maeneo hatarishi na yenye viashiria vya kuathirika na maafa na kuandaa mipango ya kuzuia madhara na kukabiliana na maafa endapo yatatokea pamoja na kuainisha na kuandaa rasilimali za usimamizi wa maafa kwa kila sekta kushiriki kikamilifu katika eneo lake.

Awali Waziri Mhagama amezikumbusha kamati hizo kuchukua hatua kwa kuzingatia utabiri wa Hali ya Hewa kwa kuelimisha wananchi kwenye maeneo yao juu ya hatua za tahadhari za kuchukua ili kuokoa maisha pale ambapo jambo lolote litatokea na kukoa mali na kutoa taarifa kwa haraka sana kwa mamlaka Husika kuhusu dalili zozote za kutokea Maafa.

Waziri Mhagama Ametoa wito kwa  wananchi wote wanaoishi na kuendesha shughuli za kiuchumi maeneo ya uwanda wa chini na pembezoni mwa mabonde ya maji wanatahadharishwa kuchukua hatua ili kunusuru maisha na mali zao.