Saturday , 26th Aug , 2023

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewasisitiza watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na ubunifu ili tija ya kazi zao iweze kuonekana kupitia huduma bora wanazozitoa.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi

Ridhiwani ameyasema hayo akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi mkoani Singida kwenye kikao kazi ambapo amewataka kufanya kazi kwa weledi na ubunifu  katika kuwahudumia wananchi.

“Ninatamani kuona utendaji kazi wenu unazingitia misingi ya maadili ya utendaji katika utumishi wa Umma kwani ndiyo msingi wa mageuzi kuelekea maendeleo endelevu vinginevyo watumishi wazembe na wenye mienendo isiyofaa kimaadili mwisho wao umefika.” alisisitiza Mhe. Ridhiwani.

Aidha, amewakumbusha watumishi hao kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anasisitiza uadilifu kazini na ametoa haki na stahiki mbalimbali kwa watumishi, hivyo, Serikali kupitia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imekamilisha mapitio, kusanifu na kuanza kujenga mifumo ya utendaji kazi Serikalini ili dhana ya wajibu pia iweze kutekelezeka kwa ufanisi.

Pia, Naibu Waziri huyo amezitaka Mamlaka za Ajira na nidhamu kuendelea kusimamia haki na stahiki zote za watumishi na kuachana na kasumba ya utendaji wa mazoea. 

Katika hatua nyingine Mhe. Ridhiwani amezitaka Halmashauri nchini kuhakikisha zinaendeleza miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF kwa kuwa ni chaguo na imeridhiwa na wananchi wenyewe katika maeneo yao. Iwapo Halmashauri na TASAF zitaunganisha nguvu ni rahisi kuwakomboa wananchi katika umaskini.

“Ninaelekeza walengwa wote wenye sifa za kunufaika na TASAF wasilipwe fedha nusu nusu kwa kuwa lengo ni kuwatoa katika wimbi la umaskini” alisema Mhe. Ridhiwani.