Tuesday , 8th Aug , 2023

Rais Samia Suluhu Hassan leo Jumanne amezindua programu ya uchimbaji wa visima kwa ajili ya wakulima wadogo 67,850 kwa nchi nzima zitakazowezesha jumla ya hekari 2,7014,000 kufikiwa na mfumo wa umwagiliaji. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan.

Akitoa maelezo kwa Rais Samia katika maonesho ya kilele cha sherehe ya wakulima Nanenane kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kila kisima kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wakulima 16.

Amesema kisima hicho kitakuwa na tenki la lita 5000 litakalokuwa limefungwa mfumo wa umeme jua (sola panel) kwa ajili ya ku-pump.

"Pia mkulima atapewa eneo la umwagiliaji la heka 2.5 na mkulima wa kwanza katika program hii anatoka wilayani Mbarali mkoani Mbeya," amesema.

Aidha, akizungumzia mradi huo, Rais Samia amempongeza Bashe kwenye eneo hilo umwagiliaji maji kwa kufanikiwa kutumia vyanzo mbalimbali ikiwamo skimu za umwagiliaji.