
Kushoto ni Ally Hamad na kulia ni mama wa marehemu
Ally alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Mount Meru, ambapo baba mzazi anataka mtoto wake akamzike mkoani Singida alipozikwa Babu wa marehemu.
"Baba yake anataka achukue mwili aupeleke Singida wakati aliniachia mtoto akiwa na miaka mitatu mpaka sasa ana miaka 30, hajui kama ana mdogo wake hajui anakula nini wala anaishije, sijajua huyu baba ana malengo gani nimemwambia aje tuongee amekataa, akasema kama nimekataa mtoto kupelekwa Singida basi tukatiane yeye achukue kichwa mimi nichukue miguu," amesema Mama wa marehemu.
Inadaiwa kuwa baba wa mtoto huyo anayejulikana kwa jina la Hamad Juma alimtekeleza mzazi mwenzake wakati mtoto akiwa na umri wa miaka mitatu pasi na matunzo yoyote lakini ghafla baba mzazi anaibuka mara baada ya taarifa za kufariki kwa kijana huyo ambapo imeelezwa kuwa baba huyo tayari amekata kibali cha kuusafirisha mwili huo kuelekea Mkoani Singida kwa ajili ya maziko.
Aidha Jitihada za kumpata Baba wa Marehemu kwa njia ya simu zilifanikiwa,ambapo alieleza kuwa endapo atanyinywa ridhaa ya kuzika mwili wa mtoto wake basi atawaachia mwili huo na hata husika na chochote kwenye msiba huo.
"Mimi nitakuwa baba mlezi kwahiyo kuna baba mzazi,na itabidi niuache kwa sababu nitakuwa nimechukia kiasi cha kutosha na sioni sababu ya kuhusika na kitu cha aina yoyote endapo watafikia hapo kwa sababu mimi nilitaka mtoto wangu nimpeleke kumzika alipozikwa babu yake," amesema Baba wa Marehemu Ally Hamad alieleza.