Thursday , 4th Jun , 2015

Mbunge wa jimbo la sengerema, william ngeleja, ametangaza nia ya kuwania urais kupitia chama cha mapinduzi (ccm) huku akieleza dhamira yake ni kuliwezesha taifa kuwa na uchumi wa kati unaojitegemea kufikia mwaka 2025.

Amesema uchumi wa kati unaojitegemea utaletwa na rais wa awamu ya tano, mwenye weledi wa kutosha, anayekerwa na umaskini wa watanzania.

Ngeleja ametangaza nia hiyo jijini mwanza mbele ya wananchi wa jiji hilo katika ukumbi wa benki kuu leo.

Ngeleja, mmoja wa makada sita wa CCM waliokuwa wamefungiwa na chama hicho Februari 18 mwaka jana kutokana na tuhuma za kuanza kampeni mapema, amewahi kuwa naibu waziri wa nishati na madini 2007 na baadaye kuwa waziri kamili katika wizara hiyo mwaka mmoja uliofuata, chini ya utawala wa sasa wa rais jakaya kikwete.

Kwa hatua yake hiyo, sasa anakuwa ni kada wa 13 wa ccm kutangaza dhamira hiyo, wengine wakiwa ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, waziri wa uvuvi na maendeleo ya mifugo, Titus Kamani, mbunge wa jimbo la Kisesa, Luhaga mpina, naibu waziri wa fedha, Mwigulu Nchemba na mtoto wa tano wa baba wa taifa, Makongoro Nyerere.

Wengine katika orodha hiyo ni balozi AIi Karume ambaye ni mtoto wa kwanza pia wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Amaan Abeid Karume, waziri wa kilimo na chakula, Stephen Wasira, waziri katika ofisi ya Rais (asiye na wizara maalum), profesa Mark Mwandosya, waziri wa zamani wa fedha katika serikali ya mapinduzi zanzibar, Balozi Amina Salum Ali, waziri wa uchukuzi, Samwel Sitta na aliyekuwa waziri wa nishati na madini, profesa Sospeter Muhongo.

Huku akijinadi kwa kutumia kauli mbiu isemayo “Maono makini, Mikakati tulivu na Matokeo halisi”, au maarufu kama ‘Tripple M’, ngeleja alisema kuwa amejipima na kujiona kuwa anayo dhamira ya kweli na anafaa kushika nafasi hiyo ya juu zaidi katika uongozi wa nchi.