Tembo
Hilo limekuja baada yakuonekana baadhi ya majina ya binadamu wanayopewa wanyama kuvutia watu wengi hali ambayo imewasukuma mamlaka hiyo kuanzisha utaratibu huo na fedha zitakazopatikana zinakwenda kuendesha shughuli za utunzaji wanyamapori na uhifadhi mali asili ya nchi.
Hayo yamebainishwa leo Jijini Dodoma na Kamishina wa Uhifadhi wa TANAPA, William Mwakilema, wakati akielezea utekelezaji wa majukumu yao na mwelekeo wa utekelezaji wa mipango kwa mwaka wa fedha 2023/24.
"Tumeanzisha utaratibu wa kuwapa majina baadhi ya wanyama lakini sio bure na hao wanyama sio wote labda kama umesema kuwa unampenda sana Fisi unataka huyo fisi awe na jina lako atapewa kwa utaratibu maalum,”amesema Mwakilema
Amesema bodi ya menejimenti ya TANAPA imeshapitisha utaratibu huo ambao utaanza na wanyama aina ya Faru.
Pia amesema mtu yoyote anaweza kufanya hivyo kama anataka hivyo ataenda kumuona mnyama husika na anaweza kumuasili na atatakiwa kuchangia gharama za kumuhifadhi mbugani shilingi milioni 1 kila mwaka.