Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Ametoa wito huo leo Julai 6, 2023, wakati alipofungua maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Polisi, Ziwani Zanzibar, na kusema kwamba Watanzania wanayo nafasi ya kufundisha Kiswahili nje ya nchi, na kuwataka kutumia fursa vizuri kwani kuna nchi tayari zimeingiza katika mitaala yao somo la Kiswahili.
"Kuwa mzawa wa lugha ya Kiswahili pekee, unakuwa hujapata fursa ya kunufaika nacho, muhimu ni kuendelea kujifunza zaidi ili kuwa mahiri, leo hii kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki Kiswahili kinazungumzwa, na hata nchi nyingine zimeingiza kwenye mpango wao somo la Kiswahili," amesema Waziri Mkuu
Amesema kuwa Watanzania wana nafasi ya kuwa walimu kwenye nchi mbalimbali ambazo zimeingiza katika mitaala yao somo la Kiswahili.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amewaagiza Mawaziri wenye dhamana na lugha ya Kiswahili, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mawaziri wa Elimu, kwa pande zote za Tanzania Bara na Zanzibar kuweka mikakati iliyo wazi ya kukuza Kiswahili na kuweka motisha kwa vijana wanaofanya vizuri shuleni.