Friday , 14th Mar , 2014

Yanga yasaka pointi 3 Jamhuri kesho

Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania bara Dar Young Africans wamesema kuwa hivi sasa wamerudi rasmi katika ligi, na wanaanza kazi katika mchezo wa kesho dhidi ya Mtibwa Sugar mchezo utakaochukua nafasi katika dimba la jamhuri mjini Morogoro.

Afisa Habari wa timu hiyo, Baraka Kizuguto, amewataka mashabiki wa timu hiyo kwenda Morogoro kuishangilia timu hiyo na kusahau matokeo ya mchezo uliopita dhidi ya Al Ahly ambapo Yanga ilitolewa kwenye michuano ya kombe la Afrika CAF kwa changamoto ya mikwaju ya penati 4-3

Kizuguto amesema kuwa si wakati wake sasa kwa mashabiki wa Yanga kutafuta mchawi au kulaumiana bali hivi sasa wanatakiwa kuwa watulivu na kuwa na umoja katika kuipa sapoti kubwa timu hiyo katika kipindi hichi ambacho ligi inaelekea ukingoni.